Breaking News

MATAIFA YA G7 YAKAMILISHA MKUTANO WAO, MZOZO WA KIBIASHARA MAREKANI NA CHINA, MOTO MSITU WA AMAZO VYATAWALA MJADALA

Kundi la mataifa saba yaliyoendelea zaidi kiviwanda G7 limekamilisha mkutano wa kilele Jumatatu baada ya kujadili changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na moto wa msitu wa Amazon na vita vya kibiashara vya Marekani
G7-Gipfel in Frankreich (Getty Images/AFP/P. Wojazer)
Mkutano huo wa kilele katika mji wa Biarritz kusini magharibi mwa Ufaransa, ghafla ulibadilika muelekeo baada ya kuwasili Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Javad Zarif kuja kujadili mkwamo wa kidiplomasia unaohusu makubaliano ya kinyuklia yaliyoafikiwa mwaka 2015.
Zarif hakuwa akitarajiwa kuhudhuria mkutano huo, lakini alialikwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye anajaribu kutuliza mvutano kati ya Iran na Marekani.
Wanadiplomasia wa Ufaransa wamesema Zarif na Trump hawakuzungumza, lakini uwepo wao katika chumba kimoja angalau umetoa matumaini.
Moto wateketeza Amazon
Katika siku ya pili na ya mwisho ya mkutano huo wa kilele, viongozi wa mataifa hayo saba ambayo ni — Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani — waligusia pia moto unaoteketeza msitu wa Amazon, ambao viongozi hao wameueleza kama shambulio dhidi ya ‘mapafu’ ya ulimwengu. Trump kwa upande wake hakuwa na mengi ya kusema juu ya suala hilo.
Viongozi wa mataifa hayo yaliyostawi zaidi kiviwanda duniani, wanaokutana katika mji wa kitalii wa pwani nchini Ufaransa wa Biarritz , wamekubaliana kutoa dola milioni 20 za dharura kuisaidia Brazil na mataifa jirani kuzuwia moto katika msitu wa Amazon.
Licha ya kwamba asilimia 60 ya msitu huo imo ndani ya ardhi ya Brazil, mataifa mengine manane ya eneo hilo yanafikiwa na msitu huo mkubwa kabisa wa asili ulimwenguni. Mataifa hayo ni Bolivia, Colombia, Ecuador, Guiana ya Ufaransa, Guyana, Peru, Suriname na Venezuela.
Suala kubwa zaidi lililodhihirisha mpasuko kati ya Trump na viongozi wengine katika mkutano huo wa G7 ni la biashara, na juhudi za rais huyo wa Marekani za kuwabania masoko hata washirika wa karibu pamoja na kuwapandishia ushuru wa bidhaa.
G7-Gipfel in Frankreich Macron und Merkel (picture-alliance/AP Photo/I. Langsdon)
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Trump aliwasili mjini Biarritz baada ya kusisitiza kuwa ataiongezea ushuru China katika wakati ambapo nchi hizo mbili zinavutana kibiashara.
Trump amuahidi biashara Johnson
Kwa mujibu wa shirika la habari la DW, Katika mkutano huo, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alikuwa mshirika wa hivi karibuni wa kundi la nchi za G7 kumsihi Trump aachane na vita vya biashara ambavyo wakosoaji wanahofia vinaweza kuuporomosha uchumi wa dunia.
Trump ametabiri kuwa Johnson atafanikiwa kuikwamua nchini yake katika mchakato wa Brexit wa Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Rais huyo wa Marekani mwenye umri wa miaka 73 amemuahidi Johnson makubaliano makubwa ya kibiashara ambayo hayakuwahi kushuhudiwa.
Halikadhalika, Trump na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe wametangaza kuafikiana juu ya makubaliano ya kibiashara ambayo wanatarajia kuyasaini mwezi ujao.
Mkutano wa pamoja wa viongozi hao na waandishi habari ambao ndiyo utafunga mkutano huo utafanyika baadaye Jumatatu.