SABABU 4 ZILIZOIMALIZA SIMBA TAIFA
SIMBA wikiendi iliyopita iliondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada kutoka sare ya bao 1-1 na UD do Songo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Matokeo haya yamewafanya Simba kuondolewa kutokana na sheria ya bao la ugenini baada ya sare ya 0-0 ugenini. Simba wameondoka baada ya msimu uliopita kufika kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, wakiwa na rekodi ya kushinda michezo yote ya mtoano nyumbani.
Hata hivyo kuna mambo mengi ambayo yalichangia timu hiyo kuondolewa, viongozi wa timu hiyo ni kati ya watu ambao wanahusika moja kwa moja kwenye adha hii ambayo imewakuta mashabiki lukuki wa timu hiyo ambao walikuwa wamejazana uwanjani:
HAKUNA MBADALA WA BOCCO: Simba walifanya usajili mzuri kwa ajili ya michuano hiyo, lakini moja ya jambo ambalo walionyesha kuwa walikuwa hawajajiandaa nalo ni kwamba kuna siku watamkosa mshambuliaji wao, John Bocco.
Kukosekana kwa mshambuliaji huyo kwenye mchezo wa wikiendi iliyopita kulionyesha kuwa Simba walikuwa wanamtegemea Meddie Kagere pekee na baada ya yeye kukabwa hawakuwa na njia nyingine.
Fedha zilizotumika kuwasajili Wabrazil watatu ambao hawajaisaidia timu hiyo na wamekuwa wakiishia benchi na jukwaani, zilikuwa zinaweza kuisaidia Simba kumpa mshambuliaji mmoja mahiri sana hapa Afrika au zilikuwa zinaweza kuwafanya Simba wakampa Okwi fedha alizokuwa anataka ili abaki kwenye timu hiyo na labda angeweza kuwasaidia.
KUJIAMINI SANA: Pamoja na kwamba Simba walikuwa wanatakiwa kucheza michezo hii miwili ya hatua ya awali ili wapate nafasi ya kwenda kwenye hatua inayofuata, lakini waliona kama vile siyo kitu sana.
Viongozi wa Simba walikuwa wanazungumza zaidi kuhusu kufika nusu fainali badala ya kuamini kuwa wanatakiwa kupenya kwanza kwa UD do Songo ndiyo wafike huko. Hii imeonyesha kuwa hawakuutilia mkazo sana mchezo huu ndiyo maana hata kutolewa kwao kumewafanya hata wenyewe washangae.
MATOKEO YA MSIMU ULIOPITA: Msimu uliopita Simba walifanikiwa kushinda michezo yote nyumbani kwao na walikuwa wanafungwa idadi kubwa ya mabao ugenini. Hii iliwafanya waamini kuwa itakuwa ni kazi rahisi zaidi kupata ushindi tena nyumbani baada ya kutoka sare ugenini.
Hii iliendelea kuwapa kiburi hata matangazo ya mara kwa mara ambayo walikuwa wakiyatoa msimu uliopita kuwataka mashabiki kwenda uwanjani hawakuyatoa kwa wingi kwenye mchezo huu wakiamini kuwa mashabiki watajaa tu kwa kuwa ni mazoea.
KIKOSI KIDOGO: Kocha wa Simba hakuwa na kikosi kipana cha kutosha kucheza mchezo mkubwa
kama huu na kilimsumbua hata kupanga.
kama huu na kilimsumbua hata kupanga.
Hii inaonyesha kuwa kikosi ambacho kocha huyo alikianzisha uwanjani hakikuwa na mbadala nje ndiyo maana hakukuwa na wachezaji bora kwenye benchi ukiachana na Hassan Dilunga. Kitendo cha Patrick Aussems kumtoa Francis Kahata na nafasi yake kuchukuliwa na Dilunga kabla ya dakika 45 za kwanza kumalizika, kilionyesha kuwa tayari kocha huyo ameshaona tatizo.
Kutokana na uhaba wa wachezaji wa kushambulia kwenye timu hiyo ndiyo maana kocha huyo aliamua kumuingiza Miraji Athuman ambaye anaonekana kabisa hakuwa kwenye mipango yake.
Lakini pia kwa kuwa kocha alikuwa anatafuta mabao na hana jinsi akajikuta akimtoa Gadiel Michael na nafasi yake kuchukuliwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambao wote ni mabeki wa pembeni. Kwa kocha ambaye ana wachezaji wengi kuanzia dakika ya sabini alikuwa anaweza kumtoa beki yeyote na kumuingiza mshambuliaji kwa kuwa ni muda wa kutafuta mabao zaidi kuliko kulinda.
Usikubali kupitwa na chochote kile tembelea App hii kila mara kupata Habari zote zinazojiri Tanzania na nje ya Tanzania katika Mapenzi na Mahusiano, Elimu, Ajira, Michezo, Maisha, Siasa na Burudani.