Breaking News

MOTO HAUFUNIKWI NA SHUKA

HALOOOO eeeehhh na utanyauka mwaka huu kama siyo kukauka kabisa! Aliyekwambia kandambili yapigwa kiwi nani? Muone jibaba zima ndevu zimejikunja kama machicha ya nazi! Heee heeeiyaaa nicheke miye mjini sikuja na kanga mwenzako nilikuja na taiti!

Unaringia makalio ya mchina wakati wenzako tuna orijino hadi huyo mchina anaulizia tunakula vitu gani! Shoga nisiseme sana mate yakanikauka maana miye naye kama hausigeli na jirani, maneno hayanikauki! Wajanja wa mjini wanakwambia pesa ni elfu kumi tu hizo nyingine zote ni chenji! Weeeeeeraaaaa!

Shoga ukiona ngedere kaja mjini jua maisha ya porini yamemshinda na miluzi mingi humpoteza mbwa, upo nyonyo! Siyo unashangaashangaa mwenzangu na mimi kumbe una nyota ya mihogo ya kukaangwa kutwa kupendwa na wanafunzi!

Jamani hivi nitumie mdomo na lugha gani ili wanawake wenzangu mnielewe?
Kwa nini lakini tumekuwa tukiitwa mzigo wa miba hatubebeki, ni kweli mwalimu wetu ni kipofu?

Wala siamini hadi leo msemo huu tena naona unatukandamiza kabisa! Shuuuutuuuu! Jamaniii! Mbona tunatia aibu tunafanya mambo hata watoto wana afadhali, ukishaharibu unakimbilia kwa waganga sasa mchawi nani kama siyo mwenyewe.

Kwa kweli nazungumza kwa uchungu, ungekuwa karibu yangu ungeona machozi yanavyonitoka. Juzi nililetewa malalamiko na mwanaume mmoja mtu mzima kwamba mkewe amekuwa mung’unya kaharibika ukubwani. Kisa na mkasa? Katika miaka zaidi ya thelathini ya ndoa yao, sasa hivi ndo kaliona penzi la nje tamu na kuifanya nyumba iyumbe. Mtu aliyenieleza namjua ana watoto watu wazima na wajukuu, bwana yule alinieleza kwa uchungu. “Hivi Anti Naa, nimuache mke wangu uzeeni watu si watasema
nina hila?” Mmh! Hilo nalo neno! Au kama watoto wa sasa watasema ni sheeda. Kwa kweli sikutaka kumjibu mwenyewe, nilifunga safari hadi kwake na kumkuta mwanamke kajaa tele kama pishi la biriani. Kwa vile nammudu nilifungua kesi mbele yao. Nilimweleza mwanaume ayaseme yote aliyosema kwangu.

Naye alirudia yote huku akiongeza na mambo yaliyokuwa ya siri ya mkewe kuondoka bila kuaga au kumpa unyumba siku anayotaka.
“Yanayosemwa juu yako ni kweli?”
“Hata yakiwa kweli wewe yanakuhusu nini?”
Majibu yake yalinichefua na kumweleza maneno ya shombo.
“Shoga kwa vile unakula dona na kushiba ndiyo maana unakuwa na jeuri ya popo kujipaka kinyesi lakini
ukiachika hakuna wa kukupa hata salamu. Siku zote ukiona kobe juu ya mti ujue kapandishwa na aliyempandisha ndiye atakayemshusha, upo nyonyo?

Acha kujitoa akili na kuzihamishia chini. Nani alikuambia hamu zinaisha kwa kutoka nje ya ndoa? Shoga ndoa mbaya kwa vile unayo lakini ukiachika utaadhirika na dunia.

Kila kitu kina wakati wake kama hukushiba kwenye sahani, utashiba kwa kujilamba? Ujana wote umeswampa hukuridhika utaridhika uzeeni?
Shuuuutuuu! Hebu acha kujitoa akili, utu uzima dawa, watoto na wajukuu wanakutegemea wewe, aliyekwambia moto unafunikwa kwa shuka nani? Leo hii wanakuona umefumaniwa na mtoto mdogo aibu iliyoje.
Acha jeuri ya nazi kushindana na jiwe, heshimu ndoa yako, heshimu umri wako siku zote ukijiheshimu utaheshimiwa, tunza heshima ya mumeo ili kila mmoja mtaani ajifunze kupitia ndoa yako.
Hebu basi jamani wanawake tubadilike, tujifunze kutokana na matukio ya wenzetu, kwa hali inayoendelea nakiri kabisa mwalimu wetu kipofu amefariki, sasa tuna mwalimu mwendawazimu. Haiingii akilini mwanamke mtu mzima kutoka nje ya ndoa na kutembea na kijana mdogo.
Mwingine nilishuhudia akifukuzwa kama mbwa baada ya kufumaniwa na mumewe kwa kuleta mwanaume ndani, jamani hii ni dharau kiasi gani kama nyumba huitaki kwa nini usiondoke kimyakimya kuliko kuondoka kwa aibu?

Narudia, mwanamke anayezipeleka akili zake chini hana tofauti na mnyama anayefanya mapenzi hadharani bila aibu. Jamani hebu tubadilike kwani nani alikufa kwa kukosa kufanya mapenzi na wanaume wengi? Hebu tutulie ili kuimarisha ndoa zetu, starehe ya siku moja inaweza kuwa aibu ya miaka mia. Nina imani nimeeleweka, kwa leo inatosha tukutane wiki ijayo.

Na Anti Nasra.

Usikubali kupitwa na chochote kile tembelea App hii kila mara kupata Habari zote zinazojiri Tanzania na nje ya Tanzania katika Michezo, Magazeti, Mahusiano, Elimu, Ajira, Video, Audios, Tamthilia na Udaku.