Breaking News

TANZANIA 1-1 BURUNDI (P: 3-0): KAULI ZA MAKOCHA BAADA YA MCHEZO, TANZANIA IKITINGA MAKUNDI


Timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imefanikiwa kutinga hatua ya makundi kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar baada ya kuisukuma nje Burundi kwa penati 3-0.

Katika mchezo wa marudiano uliopigwa leo kwenye Dimba la Taifa Dar es Salaam, timu hizo zimetoshana nguvu kwa kutoka sare ya bao 1-1 matokeo yanayofanana na yale yaliyopatikana Jumatano nchini Burundi na hivyo matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2.

Nahodha Mbwana Samatta ndiye aliyeanza kutikisa nyavu kwenye mchezo wa leo na kuitanguliza Tanzania dakika ya 29 kabla ya Abdul-razak Fieston kusawazisha dakika ya 45.

Katika hatua ya mikwaju ya penati, Tanzania imefunga penati zake zote tatu kupitia kwa Erasto Nyoni, Gadiel Michael na Himid Mao, huku Burundi wakikosa zote, mbili zikitoka nje na moja ikiokolewa na kipa wa Tanzania Juma Kaseja.

Mara baada ya mchezo kocha msaidizi wa Taifa Stars Juma Mgunda amewapongeza watanzania kwa umoja waliouonesha kuelekea mchezo huo na kuomba umoja huo uendelee kwa hatua zinazofuata.

Katika hatua nyingine, kocha Mgunda amekiri timu hiyo kuwa na tatizo la umaliziaji na ameahidi kuwa benchi la ufundi litalifanyia kazi tatizo hilo.

Naye golikipa Juma Kaseja kwa niaba ya nahodha Mbwana Samatta amesema wachezaji wa timu hiyo wanafarijika sana kwa umoja unaooneshwa na Watanzania wakiongozwa na waandishi wa habari jambo linalowafanya kuongeza mapambano wawapo dimbani.

Kuhusu kukosekana kwake kwenye timu hiyo kwa muda mrefu, Kaseja amesema haikusababishwa na kiwango chake bali huenda ni kwasababu hakuwa chaguo la makocha waliopita.

Kwa upande wake Kocha wa Burundi Allen amesema kilichowaangusha ni kukosa utimamu wa mechi (match fitness) kutokana na kuwa pamoja kwa muda mfupi.
Usikubali kupitwa na chochote kile tembelea App hii kila mara kupata Habari zote zinazojiri Tanzania na nje ya Tanzania katika Michezo, Magazeti, Mahusiano, Elimu, Ajira, Video, Audios, Tamthilia na Udaku.