FAHAMU JINSI POMBE, SIGARA ZINAVYOWEZA KUSABABISHA KISUKARI
LEO nazungumzia jinsi sigara, pombe, vyakula na mfumo wa maisha wa mtu vinavyoweza kusababisha kisukari na kuleta madhara zaidi kwa mgonjwa wa kisukari.
Kuvuta sigara kuna madhara kwa kila mtu, lakini kwa watu wenye kisukari au wanaokabiliwa na hatari ya ugonjwa huo, uvutaji sigara huwaletea madhara makubwa zaidi kiafya.
Wagonjwa wa kisukari ambao wanavuta sigara kiasi cha glucose kwenye damu zao huwa juu, hali ambayo husababisha ugonjwa huo usiweze kudhibitiwa kwa urahisi na kuwafanya wagonjwa wakabiliwe na hatari ya kupata madhara makubwa kama vile upofu, uharibifu wa neva, figo na matatizo ya moyo.
Utafiti mpya uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Polytechnics cha huko California nchini Marekani umeonyesha kuwa, nicotine inayopatikana kwenye sigara inapoingia kwenye damu ya mwanadamu, huongeza kiwango cha hemoglobin aina ya A1c kwa asilimia 34.
Mabadiliko hayo husababisha hali ya wagonjwa wa kisukari kuwa mbaya na kwa wale ambao hawana ugonjwa huo huwa katika hatari ya kupata kisukari. Jumuiya ya Kisukari ya Marekani imeeleza kuwa, imeonekana kuwa akina mama wajawazito wenye kisukari ambao wanavuta sigara, wanakabiliwa na hatari ya kujifungua watoto kabla ya muda kutimia na watoto wao kufariki dunia.
Pia wagonjwa wa kisukari wenye kuvuta sigara, hupata madhara makubwa na madogo haraka zaidi kuliko wasiovuta sigara. Kwa bahati mbaya watu wengi hudhani kuwa kwa kuwa wanaugua kisukari, ugonjwa huo utawasababishia kifo tu hata kama watavuta au kutovuta sigara, fikra ambayo si sawa.
Wagonjwa wa kisukari wanaovuta sigara, dawa za ugonjwa huo huwa haziwasaidii ipasavyo, na hivyo wanapaswa kutambua kuwa uvutaji sigara una madhara makubwa kwa afya zao. Madhara ya pombe katika kudhibiti glucose kwa wagonjwa wenye kisukari hutokea lakini hutofautiana kwa kuzingatia pombe imenywewa wakati gani na mgonjwa.
Inapaswa kufahamu kuwa, pombe inapoingia mwilini huvunjwavunjwa kama mafuta, na matokeo yake ni kupatikana kalori nyingi. Kwa ajili hiyo unywaji pombe kwa wagonjwa wenye kisukari huweza kuongeza kiwango cha glucose katika damu.
Ijapokuwa kiwango cha wastani cha pombe kinaweza kuongeza kiwango cha sukari kwenye damu, pombe inaponywewa kwa wingi hupunguza sukari kwenye damu na hata baadhi ya wakati kupungua hadi kufikia kiwango cha hatari.
Baadhi ya pombe zenye ladha tamu huongeza carbohydrates mwilini na kuongeza kiwango cha sukari kwa wingi kwenye damu. Pombe pia humuongezea mtu hamu ya kula, na kula chakula kingi huathiri kiwango cha sukari mwilini.
Baadhi ya wakati pombe huweza kuingiliana na utendaji wa dawa za kisukari hasa dawa za tembe au hata insulin. Pombe huweza kuongeza shinikizo la damu na madhara mengineyo mengi, hivyo wagonjwa wa kisukari wanapaswa kutambua kuwa pombe si salama kwa afya zao.
Kuhusiana na muundo wa maisha unavyoathiri kisukari, ni kwamba miongoni mwa mambo yanayosababisha mtu kupata ugonjwa huo ni unene wa kupindukia, kutoushughulisha mwili, chakula, mfadhaiko wa mawazo au stress na maisha ya mijini. Mafuta ya ziada mwilini husababisha wanaume wapate kisukari kwa asilimia 64 na wanawake kwa asilimia 77.
USHAURI
Kula vyakula na vinywaji vyenye sukari na mafuta huchangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ugonjwa huo. Kwa kiwango hichohicho wagonjwa wa kisukari hasa wenye kisukari aina ya pili, huweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na muundo wa maisha wanaoishi pamoja na vyakula.
Kufanya mazoezi pamoja na kutokula vyakula vyenye sukari na mafuta huweza hata kupunguza mahitaji ya insulin kwa wagonjwa wa kisukari, na kuweza kudhibiti kabisa ugonjwa huo. Kama wewe ni mvutaji wa sigara unashauriwa kuacha hasa kama una kisukari kwani sigara haina faida mwilini.
UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE