LUGOLA ACHUNGUZWA NA TAKUKURU KWA UFISADI
ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola yupo chini ya ulinzi unaomfanya asiweze kusafiri sehemu yoyote bila Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa na taarifa.
Lugola aliondolewa uwaziri baada ya kuhusishwa na kashfa ya mkataba wa Tsh. trilioni 1 wa ununuzi wa vifaa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jen. John Mbungo, alisema jana uchunguzi huo umeanza kama sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais John Magufuli aliyekabidhi suala hilo kwao kwa hatua zaidi na kuisihi mamlaka hiyo kutowaonea huruma waliohusika.
Mbungo alisema wataanza kupata nyaraka zinazohusu mkataba huo na kuhoji kila anayejua na aliyeshiriki katika mchakato wa mkataba huo, ikifuatiwa na kuwahoji watuhumiwa.
Aidha, Lugola hakuonekana katika ufunguzi wa vikao vya Bunge, jana Januari 28, 2020, jijini Dodoma, lakini leo Jumatano, Januari 29, 2020, amehudhuria.