LUGOLA AHOJIWA NA TAKUKURU MASAA 5, AFUNGUKA (VIDEO)
ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, leo Januari 31, 2020, amehojiwa kwa zaidi ya saa tano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) jijini Dodoma kufuatia agizo la Rais John Magufuli.
Kangi ambaye alitenguliwa uteuzi wake kwa tuhuma za kushiriki kuingia mkataba wa zaidi ya Tsh trilioni 1 wa ununuzi wa vifaa vya Zimamoto na Uokoaji na kampuni ya kigeni kutoka Romania, alifika TAKUKURU kuhojiwa majira ya saa 1:24 asubuhi na kutoka saa 6:35 mchana.
Akiwa ameshikilia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mkoba ulio na nyaraka, mbunge huyo wa Mwibara alishuka kwenye gari aina ya Toyota Klugger nyeusi na kuingia katika ofisi hizo zilizopo eneo la Jamhuri mjini Dodoma.
Akitoka katika chumba cha mahojiano, alipofika mlangoni alivua kitambulisho cha wageni na kuwaambia waandishi wa habari waliokuwa nje ya jengo hilo: “Habari zenu, mambo yanaendaje, mko salama, haya jamani….vipi (picha) zimetosha au bado?”
Alipotakiwa kueleza chochote kuhusu mahojiano hayo, Lugola amesema, “mimi nipo salama tu.”
Mbali na Kangi wengine ambao wanatarajiwa kuhojiwa leo kwa sakata hilo ni pamoja na aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jacob Kingu na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Yusuph Masauni.