SAMATTA AANZA KWA KISHINDO ASTON VILLA, WAICHAPA LEICESTER 2-1 (PICHA +VIDEO)
Mshambuliaji Mbwana Samatta amekuwa mtanzania wa kwanza kucheza fainali ya Carabao kwenye Uwanja wa Wembley baada ya Aston Villa kuichapa Leicester City kwa mabao 2-1 na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla 3-2.
Ushindi huo unaifanya Villa pamoja na Samatta sasa kusubiri mshindi wa mechi ya nusu fainali ya pili itakayochezwa leo Januari, 29 kati ya Manchester City dhidi Manchester United.
Katika mchezo huo Samatta akicheza mechi yake ya kwanza alifunga bao lakini mwamuzi alikataa akidai ameotea kabla ya kutolewa dakika ya 67 ya mchezo.
Wenyeji Aston Villa walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Targett dakika 22, Trezeguet alifunga bao la pili dakika 90+3, huku bao la kufutia machozi la Leicester City likifungwa na Iheanacho dakika ya 72.
Mitandao na magazeti mbalimbali ya Ulaya jana wakati yanataja nani anaweza kuanza kwenye mchezo huo na nani hataanza, Samatta alitajwa na karibia mitandao yote kuwa atacheza mechi hiyo wengi wakisema ataanzia benchi.
Awali kocha wake, Dean Smith, alisema mchezaji huyo atakuwa mmoja kati ya wale ambao wanaweza kuwafikisha kwenye hatua ya fainali.
Mchambuzi wa michezo wa gazeti la Championi, Ezekiel Kitula, ambaye ana Kolamu ya Kalamu Tamu kila Jumatatu alisema ni nadra kuona mchezaji anacheza mechi yake ya kwanza baada ya kusajiliwa tena akiwa anatoka kwenye ligi nyingine.
“Inatokeaga, lakini ni nadra sana kuona mchezaji anaanza tena kwenye mchezo mgumu wa nusu fainali, nafikiri kocha kuna kitu cha pekee amekiona na kama akicheza mchezo huo hata dakika kumi itakuwa historia nyingine kwake na kwa Watanzania.” alisema Kitula ambaye ni Mhariri wa Championi Jumatatu.