SERIKALI YAFUNGUKA ISHU YA KUZUIA MIKUTANO YA SIASA
Serikali ya Tanzania imesema utaratibu wa kuzuia mikutano ya kisiasa isiyofuata sheria na taratibu upo palepale.
Hayo yamesema jana Jumapili Januari 26, 2020 na Naibu waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni Masauni akiwa visiwani Zanzibar alipokuwa akizungumzia hali ya usalama kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2019 visiwani humo.
Alisema muda wa siasa ukifika Serikali itaruhusu mikutano hiyo yenye lengo la kutoa nafasi wa wanasiasa kuzungumza na wananchi.
“Muda wa siasa ukifika watu wataruhusiwa kuendesha mikutano mbalimbali yenye lengo la kueleza kwa wananchi walichokifanya kwa muda waliopewa nafasi baada ya kuchaguliwa na kuteuliwa katika nafasi mbalimbali,” amesema
Kuhusu hali ya usalama kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2019, amesema matukio ya mauaji yamepungua kutoka 40 mwaka 2018 hadi 35 mwaka 2019 huku akisema jitihada zimesaidia kupunguza idadi hiyo.
Amesema Serikali kupitia jeshi la polisi na mamlaka nyingine zinazohusika limeanza harakati za kudhibiti matukio hayo yanayosababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo imani za kishirikina.
Katika matukio ya udhalilishaji amesema yameongezeka baada ya matukio 35 mwaka 2019, ambapo mwaka 2018 yaliripotiwa matukio 15 na kuongeza kuwa jitihada mbalimbali zinafanyika ikiwepo utolewaji elimu kupitia askari wa Shehia na Ofisi ya Polisi Jamii na wadau.
“Matukio haya ya udhalilishaji ikiwemo kubaka, kulawiti na kunajisi Serikali tumeyaundia mkakati maalumu ikiwemo kamati maalumu iliyoundwa ikisheheni wataalamu wa udhibiti uhalifu kutoka jeshi la polisi wakiwemo wapelelezi, wataalamu wa madawati ya jinsia, tunataka kuona kadhia hiyo ya udhalilishaji inaisha Zanzibar,” amesema.
Kuhusu dawa za kulevya amesema Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kushirikiana na taasisi nyingine za ulinzi na usalama liko mbioni katika kudhibiti biashara hiyo.
“Jeshi liko makini katika kudhibiti mtandao wa biashara hiyo ambayo tumeona siku za nyuma vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa wakiharibika kwa dawa za kulevya, kuna mpango maalumu upo katika utekelezaji na tayari umeanza kutoa matokeo chanya ambapo mwaka 2019 watuhumiwa 496 wamekamatwa.”
“Tumekamata pia cocaine gramu 960.65, heroine kilogramu 10.2 na gramu 806.102, bangi kilogramu 659.6 na gramu 649.775 vijana wetu wamezamia kwenye utafunaji mirungi lakini nayo tushakamata kilogramu10.6 na gramu 096.648 pamoja na vidonge vya Valium gramu 10.30” amesema Masauni.
UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE