Breaking News

YANGA YAICHAPA PRISONS NA KUTINGA 16 BORA (ASFC)

Klabu ya Yanga SC imeungana na vigogo wenzao, Simba SC kutinga hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Yanga SC watamenyana na Gwambina FC ya Daraja la Kwanza ambayo jana iliitoa Ruvu Shooting kwa penalti 7-6 baada ya sare ya 1-1 Uwanja wa Gwambina, Misungwi.

Katika mchezo wa leo Yanga SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Luc Eymael kwa ushirikiano na gwiji wa klabu, mzawa Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ wakisaidiwa na Riedoh Berdien kutoka Afrika Kusini ambaye ni kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili na Manyika Peter, kocha wa makipa ilipata bao moja kila kipindi.





Alianza kiungo mpya Mghana, Bernard Morrison kufunga bao la kwanza dakika ya tisa kwa penalti baada ya beki Michael Ismail wa Tanzania Prisons kuunawa mpira kwenye boksi katika harakati za kuokoa krosi ya Balama Mapinduzi.

Akafuatia mchezaji mwingine mpya, mshambuliaji Yikpe Gislain Gnamien kutoka Ivory Coast aliyefunga bao la pili kwa kichwa dakika ya 63 kwa kichwa akimalizika pasi ya kiufundi ya Bernard Morrison. 

Yanga SC inaungana na Alliance FC, Ndanda SC, Ihefu FC, JKT Tanzania, Simba SC, Gwambina FC na Sahare All Stars, KMC, Panama na Mbeya City kuingia raundi ya tano ya michuano hiyo ambayo bingwa wake hucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hatua ya 32 Bora itahitimishwa kesho kwa mabingwa watetezi, Azam FC kumenyana na Friends Rangers Jijini Dar es Salaam.

UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE