Breaking News

SIMBA WATOA KIPIGO KIKALI KWA JKT TANZANIA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba SC, wameanza ligi hiyo msimu huu kwa sifa baada ya jana Alhamisi kuinyuka JKT Tanzania mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Simba ambayo wikiendi iliyopita iliondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali, ilitangaza vita mapema kwamba baada ya kuboronga kimataifa, basi msimu huu itachukua makombe yote ya ndani.

Kwa kuhakikisha hilo linafanikiwa, wameanza na ushindi huo wa jana ambapo kocha mkuu wa kikosi hicho, Patrick Aussems, alipanga watu wa kazi na hawakumuangusha.
Mfungaji bora wa ligi hiyo kwa msimu uliopita, Meddie Kagere raia wa Rwanda, ndiye aliyefungua ukurasa wa mabao baada ya kufunga bao dakika ya kwanza ambapo lilidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili, Kagere akaongeza bao la pili dakika ya 58 lililotokana na pasi ya Mzamiru Yassin Dar es Salaam kabla ya Miraji Athuman aliyeingia kuchukua nafasi ya Deo Kanda kumalizia la tatu dakika ya 73 na kuihakikisha Simba ushindi huo unaowaweka kileleni sawa na Lipuli FC.
Dakika ya 87, Edward Songo aliyeingia kuchukua nafasi ya Ally Bilal, aliifungia JKT Tanzania bao na kuwafanya kutoka uwanjani wakiambulia bao moja. Kwa jumla, mchezo ulikuwa na kosakosa nyingi katika kila kipindi ambapo dakika ya 21, mshambuliaji wa JKT Tanzania, Danny Lyanga, shuti lake kali akiwa ndani ya 18, lilidakwa kiufundi na kipa wa Simba, Aishi Manula.

Wabrazili, Gerson Fraga na Tairone dos Santos, kila mmoja kwa wakati wake alifanya shambulizi kwa kichwa langoni mwa JKT Tanzania dakika ya 27 na 39, lakini mashambulizi hayo hayakuzaa matunda.

Ibrahim Ajibu, ilibaki kidogo aifungie Simba bao la nne dakika chache kabla ya mchezo kumalizika, lakini alishindwa kuukontroo mpira aliopewa na Mzamiru ndani ya 18. Mara baada ya mchezo kumalizika, Aussems, alisema: “Tulifahamu kwamba mchezo utakuwa mgumu na hatukuwa tayari kuona tunapoteza.

“Lakini kila muda ulivyokuwa unakwenda uhakika wa ushindi ulikuwa upande wetu na tulikuwa na uhakika wa kufunga mabao si chini ya sita, uzembe wetu ndiyo umefanya tumefunga mabao haya.
Tutayafanyia kazi mapungufu hayo yasijirudie tena.” Upande wa Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed ‘Bares’ alisema: “Nimeridhika na matokeo haya, makosa ya walinzi wangu ndiyo yametugharimu. Sasa tunakwenda kujipanga kwa michezo ijayo

Na Ibrahim Mussa, Dar es Salaam

Usikubali kupitwa na chochote kile tembelea App hii kila mara kupata Habari zote zinazojiri Tanzania na nje ya Tanzania katika Mapenzi na Mahusiano, Elimu, Ajira, Michezo, Maisha, Siasa na Burudani.