Breaking News

FAILI LA BURUNDI LAFUNGWA LA SUDAN LAFUNGULIWA, MASHABIKI WAITWA TENA

BAADA ya kazi kubwa iliyofanywa na Taifa Stars Jumapili ilipocheza dhidi ya Burundi mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),limeanza mikakati mipya ya kuona timu inafanya vema dhidi ya Sudan hivi karibuni.

Taifa Stars itapambana na Sudan katika mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kuwapongeza wanakamati wote waliohusika katika kuhamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuiunga mkono Taifa Stars dhidi ya Burundi iliyofanyika katika Hoteli ya Seacliff jijini Dar, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau amesema kuwa mikakati kwa ajili ya mchezo dhidi ya Sudan tayari imeshaanza.

 “Kwanza kabisa niwapongeza mashabiki kwa kazi kubwa ya kuiunga mkono Taifa Stars waliyoifanya dhidi ya Burundi, hakika ilikuwa ni ya aina yake na ambayo sikuwahi kuiona.
“Hata hivyo, baada ya mechi hiyo sasa tunajipanga kwa ajili mechi yetu ijayo ya Chan dhidi ya Sudan ambayo tutashiriki hivi karibuni.
“Tukifanikiwa kuwatoa Sudan basi tutakwenda katika fainali hizo na tutakuwa tumeandika historia ya kushiriki fainali zote kubwa za Afrika ndani ya kipindi kifupi,” amesema Kidau.

Katika hatua nyinge, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Hamasa ya Taifa Stars, Haji Manara amesema: “Kwa upande wetu tumejipanga vilivyo kwa ajili ya kutimiza majukumu yetu lakini pia niwaombe tu Watanzania wote kuendeleza utamaduni wa kuja kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kuiunga mkono timu yetu ya taifa.

“Tulichofanya dhidi ya Burundi basi kiwe mara mbili zaidi tutakapokutana na Sudan hivi karibuni katika Uwanja wa Taifa," amesema.

Usikubali kupitwa na chochote kile tembelea App hii kila mara kupata Habari zote zinazojiri Tanzania na nje ya Tanzania katika Michezo, Magazeti, Mahusiano, Elimu, Ajira, Video, Audios, Tamthilia na Udaku.