Breaking News

CHAMA AKALIA KUTI KAVU SIMBA

TAA nyekundu imemuwakia kiungo mchezeshaji wa Simba, Clatous Chama, raia wa Zambia ambapo anaweza kuwa mmoja ya wachezaji ambao watapigwa panga katika dirisha dogo la usajili kutokana na kumezwa na starehe za Jiji la Dar es Salaam.

Inaelezwa kuwa Chama amekuwa na mambo mengi nje ya uwanja ambayo yamesababisha kushindwa kuwa na msaada mkubwa kwa Simba kama ilivyokuwa awali.

Chama alitua Simba msimu uliopita akitokea Power Dynamos ya Zambia ambapo alikuwa moto na kusaidia timu hiyo kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Katika siku za karibuni, kiungo huyo ameshuka kiwango ambapo hata katika mechi ya juzi Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting hakuwepo kikosini.

Habari zisizo na shaka ambazo Championi Jumatatu, limezipata ni kuwa kiungo huyo ameshuka kiwango kutokana na kutofanya mazoezi inavyotakiwa na badala yake amekuwa akitumia muda mwingi kwa ajili ya starehe za nje ya uwanja.

“Chama kwa sasa viongozi wanajadili juu ya uwezo wake kwa sababu ameshuka sana tofauti na wakati ule ambao alitua akitokea kule kwao.

“Hafanyi mazoezi vile ambavyo inatakiwa ndiyo maana unaona uwezo wake kwa sasa umepungua sana ikiwa ni tofauti na mwanzoni. Amekuwa mtu ambaye anafanya sana starehe za nje ya uwanja na ndizo ambazo zinachangia uwezo wake kushuka.

“Kwa sasa yupo katika wakati ambao viongozi wanamjadili na kama akiendelea hivi kuna hatari ya kuachwa katika dirisha dogo la usajili kwa sababu haonyeshi tena uwezo ule ambao alikuwa nao mwanzo,” kilisema chanzo hicho ambacho ni mmoja wa vigogo wakubwa Msimbazi.

Championi Jumatatu, lilimtafuta Katibu wa Simba, Dk Anord Kashembe juu ya ishu hiyo na kusema: “Kuna kamati ya usajili ambayo inadili na kila kitu juu ya masuala hayo. Siwezi kulitolea ufafanuzi zaidi.”

CHANZO: CHAMPIONI.
UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE