Breaking News

MATOKEO YA MICHEZO YA LIGI KUU TANZANIA BARA NOVEMBER 25,2019

TANZANIA Prisons imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Shujaa wa Prisons inayofundishwa na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Mohammed ‘Adolph’ Rishard ni mshambuliaji wake, Adili Buha aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 25.

Na kwa ushindi huo, timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza nchini, Prisons inafikisha pointi 20 katika mchezo wa 12 na kupanda hadi nafasi ya tatu, nyuma ya Kagera Sugar pointi 23 za mechi 11 na mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 25 za mechi 10.

Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Namungo FC wamezinduka baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, bao pekee la Bigirimana Blaise dakika ya 32 Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Baada ya ushindi huo, Namungo FC ambayo kama Polisi zimepanda Ligi Kuu msimu huu, inafikisha pointi 19 katika mchezo wa 12 na kupanda hadi nafasi ya nne, wakati wapinzani wao wa leo wanabaki na pointi zao 16 za mechi 11.

Na bao pekee la Deogratius Anthony dakika ya 88 limetosha kuipa Coastal Union ya Tanga ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 

Kwa ushindi huo, Coastal Union ya kocha Juma Mgunda inafikisha pointi 17 baada ya kucheza mechi 12 ikipanda nafasi ya sita nyuma ya Lipuli FC yenye pointi 18 za mechi 11, wakati Ndanda FC inabaki na pointi zake saba za mechi 11 katika nafasi ya 19 kwenye ligi ya timu 20.
UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE