RASMI TANZANIA YAPOTEZA NAFASI NNE ZA CAF
Tanzania imepoteza rasmi fursa ya kuwakilishwa na timu nne katika mashindano ya klabu Afrika kufuatia timu ya Al-Nasr ya Libya jana kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Djoliba ya Mali.
Bao pekee lililopachikwa na mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, Moataz Al-Mehdi katika dakika ya 68 lilitosha kuipa ushindi Al-Nasr ambao uliifanya ifikishe pointi nane ambazo ziliihakikishia rasmi kutinga hatua ya robo fainali ikiwa imeshika nafasi ya pili katika kundi C nyuma ya vinara Horoya ya Guinea ambao wana pointi 11.
Kitendo hicho kimeifanya Libya kufikisha jumla ya pointi 16.5 na kuingia katika kundi la nchi 12 ambazo kila moja ina fursa ya kuingiza klabu nne katika mashindano ya klabu Afrika kwa msimu wa 2020/2021 na kuipiku Tanzania ambayo yenyewe hadi sasa ina pointi 14 katika mfumo wa ukokotoaji alama za klabu kutokana na ushiriki wa timu za nchi husika katika mashindano ya klabu unaosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).
Al-Nasri wanafuzu hatua ya robo fainali licha ya Djoliba kuwa na uwezekano wa kufikia pointi walizonazo kutokana na wapinzani wao hao wanaoshika nafasi ya tatu kuwa na pointi tano kwa sasa, lakini timu hiyo ya Libya inanufaika na kanuni ya kuwa na matokeo mazuri dhidi ya timu hiyo ya Mali kwani walitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza nyumbani kabla ya kuibuka na ushindi huo wa ugenini jana.
Tanzania inaweza kuporomoka zaidi hadi nafasi ya 14 katika viwango hivyo vya ufanisi wa klabu za nchi husika katika mashindano ya klabu Afrika ikiwa timu ya San Pedro ya Ivory Coast itamaliza katika nafasi ya tatu ya kundi D la mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Kwa sasa Ivory Coast ina pointi 13.5 na ikiwa San Pedro itamaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi lake, pointi za nchi hiyo zitaongezeka na hivyo itapanda kutoka nafasi ya 14 hadi ya 13 ilipo Tanzania.
Ifahamike kwamba kitendo cha timu nne zilizoiwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika msimu huu kushindwa kutinga hatua ya makundi, kimechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa pointi za Tanzania na kupoteza fursa hiyo kwani pointi hizo zimekuwa zikihesabiwa kuanzia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Simba iliishia hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutolewa na UD Songo ya Msumbiji wakati Yanga ilikwama mbele ya Zesco United katika raundi ya kwanza ya mashindano hayo na hata ilipoangukia katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilikwama mbele ya Pyramids FC ya Misri.
Kwa upande wa Azam FC yenyewe ilikomea katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya Triangle United ya Zimbabwe na KMC ilitolewa na AS Kigali ya Rwanda katika hatua ya awali ya mashindano hayo.
Credit: Mwanaspoti
UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE