Breaking News

SPORTPESA YAINGIA MKATABA NA NAMUNGO FC


KAMPUNI ya ubashiri ya SportPesa imeingia mkataba wa udhamini wa mwaka mmoja na Namungo FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza kwa niaba ya SportPesa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SportPesa Tarimba Abbas alisema, nia ya SportPesa ni kuendeleza soka la Tanzania na kuongeza ushindani miongoni mwa timu za ligi.

“Nadhani mnakumbuka siku zote tumekuwa tukisema SportPesa imekuja Tanzania kwa nia ya kuendeleza sekta ya soka, ndiyo maana tuliingia mikataba na klabu kubwa na kongwe za Simba, Yanga na Singida United. Pia tulitoa sapoti ya kifedha na vifaa vikiwemo jezi kwa timu ya Polisi Tanzania vitu ambavyo vimekuwa chachu kwa wao kuingia ligi kuu”alisema Tarimba.

Tarimba aliongeza kuwa wanaimani kubwa na Namungo ambayo ipo nafasi ya tano kwenye ligi na ndiyo maana wameamua kuweka udhamini huo wakiamini wanaweza kufanya vizuri na kutoa upinzani msimu huu na ujao.
Mkataba wa udhamini wa SportPesa na Namungo wa mwaka mmoja na utakuwa na thamani ya Sh Mil 120.


Kwa upande wa Namungo, Mwenyekiti wa timu hiyo Hassan Zidadu aliwashukuru SportPesa kwa udhamini huo na kuahidi kutumia fursa hiyo vizuri kutimiza malengo ya wadhamini hao.

“Tunawashukuru sana SportPesa kwa kutupa fursa hii kwa timu yetu na tunatoa ahadi ya kufanya vyema ili tuchukue ubingwa wa ligi au Kombe la FA ili tuweze kuitangaza chapa ya SportPesa kimataifa” Alisema Hassan.

UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE