Breaking News

YANGA KUKIPIGA NA KMC KESHO

Katika kujiandaa na mchezo wake wa kiporo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mwadui FC June 13 kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga, Klabu ya Yanga SC itakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Yanga inataka kuutumia mchezo huo kujua hali halisi ya kikosi chake kabla ya kumenyana na Mwadui FC huko Shinyanga wiki ijayo na baadaye JKT Tanzania Dar es Salaam.

Wiki iliyopita Bodi ya Ligi ilitoa ratiba ya mechi za viporo za Ligi na siku moja baada ya Yanga kumenyana na Mwadui, mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting June 14 kwenye Uwanja wa Taifa.

Mechi nyingine ya June 13 ni kati ya Coastal Union FC na Namungo FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga, wakati June 14, Azam FC nao watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na June 17, Yanga SC watakuwa wageni wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Taifa.

Baada ya kukamilisha mechi hizo za viporo, rasmi Ligi Kuu itaanza June 20 na kufikia tamati July 26, mwaka huu baada ya kusimama tangu March 17, mwaka huu kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona duniani kote.  

Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza Ligi kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.

Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.