ALIYETUHUMIWA KUBAKA NA KULAWITI WAKE ZA WATU, AFUNGULIWA KESI YA UHUJUMU UCHUMI
Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga, amesema ofisi yake imemfungulia mashtaka ya uhujumu uchumi, Ahmed Abdulkarim Mohamed kutokana na makosa ya kuwalaghai wanawake na kuwaingilia kimwili bila matakwa yao.
Akizungumza na wanahabari Jana Jijini Dar es Salaam, DPP Mganga amesema kuwa Bwana Ahmed amekuwa akiwarubuni wanawake ambao wengi ni wake za watu na wenye familia zao kwa minajili ya kufanya nao biashara, kisha kuwawekea madawa na kuwaingilia kimwili na wengine kinyume na maumbile.
Wakati wa akifanya ufusika huo, Mtuhumiwa amekuwa akiwapiga picha na kurekodi video ambazo baadae huzitumia kuwatisha na kuwadai fedha ili asizi-posti kwenye mitandao ya kijamii.
Amekuwa akiwatisha akijua kuwa ni watu wenye heshima, waume na familia zao hawatakubali kuruhusu picha zao zisambae mitandaoni, Hivyo amekuwa akilipwa kiasi cha fedha anachotaka.
“Huyu jamaa amekuwa akiwarubuni kina mama wenye uwezo pamoja na raia wa kigeni, akishakutana nao anawalewesha kwa dawa kisha kuwabaka na kuwaingilia kinyume na maumbile, tayari waathirika ni wengi ambao tunawaomba wajitokeze,”ameeleza DPP.
Alisema kutokana na aina ya vitendo walivyofanyiwa, kesi dhidi ya mtuhumiwa iliyofunguliwa Agosti 21, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itasikilizwa kwa faragha na haitaruhusiwa watu wengine kuwepo zaidi ya mtuhumiwa na walalamikaji.
DPP Mganga amesema tayari walalamikaji watano wamejitokeza na kuna idadi kubwa zaidi ya walalamikaji ambao anawahakikishia kuwapo usiri iwapo watajitokeza ili kutoa ushahidi dhidi ya mtuhumiwa huyo.
Alidai mtuhumiwa amekuwa akitumia majina tofauti ya watu maarufu, likiwemo la Ahmed Abdulkarimu Mudhihir na wakati mwingine amewahi kujiita Mwamvita Makamba na amekuwa akifanya utapeli huo kwa wanawake wenye familia zao.
DPP amesema awali, Mtuhumiwa alipelekwa Mahakama ya Kindondoni, lakini aliachiwa kwa dhamana na aliendelea kutekeleza uhalifu huo, hivyo alipobaini kuhusu tuhuma zake kwa kuwa anawajibika kulinda usalama na haki za watu na kuhakikisha hakuna anayebughudhiwa, aliamua kumfungulia mashtaka hayo ya uhujumu uchumi.
“Kutokana na vitendo vya kutumia picha za walalamikaji kuwadai fedha na anadaiwa kuiba fedha kwa baadhi ya walalamikaji, hivyo tumemfungulia kesi hiyo namba 85 ya uhujumu uchumi ambayo inaambatana na kesi namba 83 na 69 ya utakatishaji fedha na kesi hizi zote ziko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,” amesema DPP.
Chanzo: Gazeti Mtanzania.