Breaking News

DANTE NA YANGA HAKUJAELEWEKA BADO


Baada ya kushindwa kufikia makubaliano na uongozi wa Yanga kuhusu malipo ya madai yake, beki Andrew Vicent 'Dante' au Chikupe amesema kuwa hatma yake itafahamika katika dirisha dogo la usajili.

Tangu kuanza kwa msimu huu Dante 'alijiondoa' Yanga akishinikiza alipwe malimbikizo ya madai ya fedha za usajili zaidi ya Tsh Milioni 50.

Beki huyo aliyeitumikia Yanga kwa mafanikio katika misimu mitatu, amesema hakuna mwafaka uliofikiwa kati yake na Yanga.

"Nilianza kufanya mazungumzo vizuri na uongozi lakini badae tukashindwa kuelewana," amesema

"Ila bado naendelea kuwasikilizia hadi hapo dirisha dogo litakapofunguliwa ndio nitafahamu hatma yangu"

Yanga huenda ikalazimika kuvunja mkataba wa beki huyo kwani kwa zaidi ya miezi minne hayupo kazini.

Aidha kwa upande wa Dante ni kama hayuko tayari kuendelea kucheza Yanga kwani uongozi wa timu hiyo ulikubali kumlipa fedha zake kwa awamu tatu lakini alikataa akitaka alipwe fedha zote kwa mkupuo.


Nyota wengine waliokuwa na madai akiwemo nahodha Msaidizi Juma Abdul walikubali kupokea malipo yao kwa awamu na kuridhia kurejea kikosini hapo.
UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE