Breaking News

KILIMANJARO QUEENS YAANZA KWA KISHINDO KIKUBWA CECAFA CHALLENGE

WENYEJI, Tanzania Bara au Kilimanjaro Queens wameanza vyema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Wanawake baada ya ushindi wa 9-0 dhidi ya Sudan Kusini jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.

Kila mchezaji wa Kilimanjaro Queens, mabingwa mara mbili mfululizo wa michuano hiyo aling’ara siku ya leo, lakini heshima ya nyota wa mchezo huo wa Kundi A inaweza kwenda kwa Mwanahamisi Omar Shaluwa ‘Gaucho’ ambaye amefunga mabao matatu peke yake.

Mwanahamisi aliyejiunga na Simba Queens msimu huu kutoka Mlandizi Queens, amefunga mabao yake katika dakika za 18, 43 na 47 wakati mengine yamefungwa na Deonisia Minja dakika ya 33, Opa Clement Sanga dakika ya 50 na 88, Stumai Abdallah dakika ya 48 na 52 na Julitha Singano dakika ya 55.



Katika mchezo uliotangulia wa Kundi A, Burundi iliichapa Zanzibar 5-0 mabao yake yakifungwa na Sakina Saidi dakika za 24 na 35, Sandrine Niyonkuru dakika ya 55, Aziza Hajji aliyejifunga dakika ya 86 na mtokea benchi Aniela Umimana dakika ya 88.

Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi za Kundi B, Ethiopia wakimenyana na Kenya kuanzia Saa 10:00 jioni na Uganda wakimenyana na Djibouti kuanzia Saa 12:00 jioni
UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE