MARADONA AENDELEZA SINEMA ZAKE KWENYE SOKA
Diego Maradona ameendelea sinema zake kwenye mchezo wa soka baada ya kujiuzulu kisha saa 48 baadaye akaamua kufanya maamuzi tofauti kwa kurejea katika majukumu ya ukocha katika timu ya Gimnasia.
Siku tatu zilizopita Maradona ambaye amekuwa na vituko vya mara kwa mara kwenye soka, alitangaza nia yake ya kujiondoa kwenye timu hiyo.
Lakini taarifa zilizotoka jana zinaeleza kuwa kocha huyo sasa anatarajiwa kuiongoza timu yake ya Gimnasia katika mchezo dhidi ya Arsenal de Sarandi, kesho Jumapili.
Mwanasheria wa Maradona, Matias Morla amesema mteja wake ataendelea na kazi kwa kuwa ameshawishiwa kubaki.
Mashabiki walifika nyumbani kwake na kumuomba kutoondoka, walimsisitiza kubadili maamuzi yake, baada ya kupata taarifa kuwa ataendelea na kazi waliibuka na shangwe kubwa.
Baada ya kutangaza nia yake ya kuondoka kwenye timu, Maradona alitarajiwa kukutana na rais wa klabu yake, Gabriel Pellegrino lakini sasa mkutano huo hautakuwa ni kuhusu kufukuzana tena.
Wakati sarakasi hizo zikiendelea Gimnasia haijatoa tamko rasmi juu ya majaaliwa ya Maradona laki taarifa za ndani zinaeleza kuwa muda wowote wanaweza kutoa tamko.
Kwa sasa Gimnasia inashika nafasi ya 22 katika timu 22 baada ya mechi 13 za msimu huu wa 2019/20 katika Ligi Kuu ya Argentina.
UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE