YAFAHAMU MADHARA YA WAPENZI KUGOMBANA NA KUNUNIANA MARA KWA MARA
MADHARA Karibu tena katika ukurasa huu mzuri. Wiki iliyopita tuliianza mada hii kama inavyojieleza hapo juu. Nilianza kwa kukupa ushuhuda wa mmoja kati ya wasomaji wangu, dada yetu ambaye yupo kwenye wakati mgumu sana akihitaji msaada wa kimawazo kutoka kwetu.
Suala lake kwa kifupi ni kwamba, alikuwa na kawaida ya kugombana mara kwa mara na mumewe kisha wananuniana kwa muda mrefu, mwisho akajikuta akiingia katika mtego hatari wa kumsaliti mumewe. Tatizo linakuwa kubwa zaidi kwa sababu anaonesha kuanza kuzama kwenye penzi la mchepuko!
Nakushukuru msomaji wangu ambaye umenitumia ujumbe wa kumshauri dada yetu huyu, meseji zilikuwa ni nyingi na zenye ujumbe maridhawa, niseme tu kwamba mchango wako ni wa muhimu sana.
Tukija kwenye hoja yetu ya msingi, ushauri ambao wengi wenu mmeupendekeza na ambao ndiyo hasa unaomfaa dada huyu, ni kwamba alifanya makosa makubwa kwa kumsaliti mumewe na hata kama mume ndiye aliyekuwa sababu ya yeye kufanya dhambi hiyo, bado ukweli unabaki palepale kwamba amefanya kosa kubwa sana.
Wakati mwingine ni vyema kuendelea kukumbushana kwamba katika uhusiano wa kimapenzi, kosa pekee ambalo huwa halisameheki huwa ni usaliti! Hata vitabu vya dini zote vinaeleza kwamba usaliti ni kosa pekee linaloweza kumpa mtu nguvu ya kutoa au kudai talaka!
Hii maana yake ni kwamba usaliti haukubaliki hata kidogo, iwe umefanya kwa bahati mbaya, mumeo au mkeo ndiyo aliyesababisha usaliti, ukweli unabaki palepale, usaliti ni kosa linalostahili kuvunja kabisa uhusiano wowote, hata kama mlikuwa mmefika mbali kiasi gani.
Anachotakiwa kufanya dada huyu, ni kuachana mara moja na dhambi hiyo ya usaliti, ajutie ndani ya nafsi yake na ajiwekee nadhiri ya kutokuja kufanya kosa kama hilo tena.
Lakini kwa wewe mwenye tabia ya kugombana mara kwa mara na mwenzi wako kisha unaacha muda mrefu upite katikati yenu, tambua kwamba unachimba shimo ambalo ni wewe mwenyewe ndiye utakayekuja kuingia.
Kugombana ni suala la kawaida kabisa katika uhusiano wa kimapenzi, hakuna wanandoa au wapenzi ambao huwa hawagombani lakini ikishatokea kwamba mmetofautiana, ni jukumu lenu nyote kuhakikisha kwamba mnamaliza haraka tofauti zenu ili maisha yaendelee.
Kubali kujishusha hata pale unapoona kabisa kwamba mwenye makosa siyo wewe. Acha mambo yapite na maisha yaendelee, tabia ya kujiona upo sahihi kila mara, ndiyo inayofanya wengi wawe wanagombana mara kwa mara, hata kwa yale mambo ambayo ni madogo na ya kawaida sana.
Unapokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi, tambua kwamba jukumu lako la kwanza ni kushughulikia furaha ya mwenzi wako. Fanya kila unachoweza kuhakikisha anakuwa na tabasamu kwenye uso wake. Ukiona kila mara anakununia, tambua kwamba kuna mahali unafeli na lazima ushughulikie hapo unapofeli haraka ili kuepusha madhara mengine makubwa ambayo yanaweza kuzuilika.
Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
UPDATE NIJUZE HABARI APP, CLICK HERE