NILIVYOTAMANI KUMCHARAZA BAKORA VERASIDIKA
MIAKA ya nyuma kidogo nilipata kumfahamu mwanadada kutoka Kenya mwenye kalio kubwa sana na akawa analitumia kujitafutia umaarufu. Mdada huyu alifahamika kwa jina la Corazon Kwamboka. Ni msichana aliyeumbika kisawa-sawa, watoto wa mjini wanasema alijaaliwa figa namba nane.
Kilichombeba zaidi mdada huyu ni kwamba kwenye ile nane yake, duara la chini lilikuwa kubwa zaidi, yaani ndiyo kusema kwamba alikuwa na msambwanda wa kuweza kumtikisa mwanaume yoyote aliyekamilika.
Nikashawishika kumjua zaidi na ndipo nilipoingia kwenye ukurasa wake Instagram. Huko nilikutana na picha zake kibao akiwa amejiachia! Picha nyingi zilikuwa za nusu utupu. Sehemu kubwa ya mwili wake ilikuwa wazi.
Hapo ndipo nilipoanza kumfuatilia dada huyu kujua anafanya nini na kwa nini anafanya hivyo. Nikaja kugundua kuwa Corazon ni mwanasheria kitaaluma na alijiingiza kwenye mambo ya uanamitindo baada ya kuona shepu yake inamruhusu. Katika kuendelea kumchimba Corazon, ndipo nilipokuja kukutana na mwanadada mwingine aliyefahamika kwa jina la Vera Sidika Mung’asia.
Vera Sidika kwenye mitandao mbalimbali alikuwa akitambulishwa kama mwanamitindo na staa mkubwa nchini Kenya lakini tabia zake hazikuwa tofauti na za Corazon. Kama ilivyokuwa kwa Corazon, Vera Sidika naye alikuwa mtaalam wa kupiga picha chafu. Naye alikuwa amejaaliwa kalio kubwa, akawa analitumia kuwachanganya wanaume kwa kulianika mitandaoni.
Mara kadhaa wawili hao wamekuwa wakipambanishwa sambamba na mwanadada Mbongo, Jane Ramoy ‘Sanchi’ lakini Vera na Sanchi walionekana kufunikana. Hata hivyo warembo hao wote wamekuwa wakitafunwa na skendo ya kutumia dawa za Kichina.
Tuachane na historia za wadada hao, nirudi kwenye tukio la hivi karibuni ambalo ndilo lililonisukuma kuandika makala haya. Mwishoni mwa wiki iliyopita ulimwengu wa burudani uligubikwa na tukio kubwa la baby shower ya mpenzi wa staa mkubwa wa muziki Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tanasha Donna.
Kwenye sherehe hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Western Coral Beach iliyopo Masaki jijini Dar, walihudhuria mastaa kibao na yalitikisa matukio mengi lakini staa aliyeacha gumzo zaidi ni mwanadada Vera Sidika.
Vera ambaye ni shosti mkubwa wa Tanasha alitinga kwenye sherehe hiyo akiwa amevalia nguo iliyoacha maungo yake wazi kiasi cha kuwafanya hata wale micharuko wa mjini kupigwa na butwaa. Hebu vuta picha, Vera Sidika yule ambaye ni kati ya mastaa wenye shepu kubwa Afrika Mashariki, anatinga ukumbini akiwa amevalia nguo ya ndani tu, aibu iliyoje!
Halafu sasa, mwenyewe wala hakuwa akiona aibu. Alikuwa akikatiza mbele za watu kwa kujishaua, na hata pale alipotakiwa kupozi kwa ajili ya kupiga picha, aliweka mapozi kama yote. Unabaki ukijiuliza, alikuwa amelewa sana, alikuwa akitangaza biashara au aliamua tu kutafuta kiki kupitia shughuli hiyo? Mpaka leo mimi sina jibu na niwaambie tu kwamba, siku ile nilitamani ningekuwepo pale ukumbikini niandike historia ya kumuadabisha kwa kumcharaza bakora.
Ndiyo! Ningefanya hivyo kwa lengo ya kutoa fundisho kwa wengine. Niseme tu kwamba, alichokifanya mwanadada huyo ni kitendo cha aibu ambacho hakistahili kuigwa na staa yoyote wa Bongo. Najua tunao micharuko wetu lakini sijawahi kuona ambaye amefanya kama alivyofanya Vera. Angalizo langu ni kwa mastaa kama vile Irene Uwoya ambaye naye alitinga na gauni ambalo lilikuwa likionesha nguo yake ya ndani.
Huo siyo utamaduni wetu jamani. Sasha, Sanchi, Wema, naongea na nyie. Kamwe msidhubutu kufanya kile alichofanya Vera, mkiiga kwa ulimbukeni wetu nawahakikishia hamtabaki salama kwa Tanzania ya sasa. Igeni yote lakini siyo haya mambo ya kipuuzi ambayo yatawashushia heshima mbele ya jamii. Mimi nimeweka nukta, nimeona hili lisinipite hivihivi maana lilinichefua kupita maelezo.